Ridhiwani akihutubia Waandishi asubuhi ya leo Kiromo Hotel |
mkutano wa (TASWA)Bagamoyo
MWENYEKITI
wa Kamati ya Kusaidia timu za soka za vijana za taifa, Ridhiwani Kikwete,
amesema mfumo wa uendeshwaji wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam ni mbovu kwa
sababu unategemea mfuko wa mtu mmoja.
Akizungumza wakati
anatoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari
za Michezo Tanzania (TASWA), Hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani Pwani, Kikwete alisema kwamba Yanga inahitaji kubadilika
kutoka mfumo huo.
Kikwete alisema
ni afadhali mfumo wa uendeshwaji wa Simba SC, ambao desturi yao ni
kuchangishana.
“Nilijaribu
kufanya uchunguzi wa mfumo wa uendeshwaji wa klabu ya Yanga, nikashangazwa ni
mfumo mbaya, kwa sababu unategemea mfuko wa mtu mmoja, afadhali Simba wao huwa
wanachangishana,”alisema.
Ingawa hakumtaja
mtu ambaye mfuko wake unategemewa Yanga, lakini wazi ni Mwenyekiti wa klabu hiyo,
Alhaj Yussuf Mehboob Manji.
Kwa ujumla katika
hotuba yake, Kikwete alisema haridhishwi na mfumo wa uendeshwaji wa soka ya
Tanzania na kwamba unahitaji mabadiliko.
Kikwete aliushauri
uongozi wa TASWA upiganie nafasi ya uwakilishi ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) na kusisitiza juu ya umuhimu wa waandishi nchini kutambua haki zao.
Lakini pia
Kikwete aliwaasa waandishi kuepuka uandishi wa kinazi wa Simba na Yanga na
badala yake kuzama ndani zaidi katika kuripoti, sambamba na kuripoti michezo yote,
badala ya kuegemea kwenye soka pekee.
“Vyombo vya
habari lazima viwe na wataalamu tofauti wa kuripoti michezo tofauti, huyu
akiegemea kwenye soka, mwingine aegemee kwenye mchezo mwingine, ili kuhakikisha
tunafikisha ujumbe vema kwa jamii,” alisema mtoto huyo wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Ridhiwani ambaye
pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya
CCM, NEC akiiwakilisha Wilaya ya Bagamoyo alisema kwamba ipo haja ya TASWA
kuendesha semina kadhaa za kuelimisha Waandishi wa Habari kuweza kuripoti
michezo mbalimbali nchini.
Aidha,
katika mkutano huo, wanachama walielimishwa kuhusu uanzishwaji wa Saccos na
kuridhia kuanza kwa mchakato wa kuundwa kwa chama cha ushirika wa akiba na
mikopo kwa Taswa. Walipendekezwa wajumbe waunde timu ya mpito.
No comments:
Post a Comment