Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig |
Na Doris Maliyaga, Muscat
HII Simba bwana wacha tu. Imetia Oman ikiwa na wachezaji wanane lakini kama imekamilika na inaendelea na taratibu zake kama kawaida, huku kocha akiwataka wachezaji kucheza mchezo wa haraka haraka. Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig ili kutimiza azma yake amehakikisha anaongeza stamina kwa nyota wake.
Mfaransa huyo amekuwa akiwatawanya wachezaji uwanja mzima mazoezini pamoja na ukweli kuwa wachezaji ni wachache. Kutokana na wachezaji hao kuhaha uwanja mzima, kwa kiasi kikubwa inawasaidia kuongeza pumzi.
Liewig amesisitiza kuwa malengo yake ni kuona timu ikicheza mchezo wa pasi na kasi mithili ya Barcelona ya Hispania. Katika mazoezi ana wachezaji saba ambao ni Felix Sunzu, Haruna Moshi 'Boban', Haruna Shamte, Ramadhani Chombo 'Redondo', Kigi Makassy, Salim Kinje na Nassor Said 'Cholo'.
Kipa Abel Dhaira kutoka Uganda alikuwa na tatizo la ngozi lakini amepona na anatarajiwa kuanza mazoezi leo Jumamosi. Dhaira inadawa alikuwa hawezi kuvaa viatu vya kuchezea kutokana na tatizo hilo.
Akizungumza na Mwanaspoti daktari wa timu, Cosmas Kapinga alisema: "Kutokana na maendeleo yake tunatarajia kesho (leo Jumamosi) ataanza mazoezi na wenzake." Akizungumzia tatizo hilo, Dhaira alisema:"Tatizo hili linaninyima raha kwani malengo yangu ni kucheza mpira na si kukaa nje."
Tatizo hilo inadaiwa lilitokea kutokana na kuchanganya hali ya hewa sehemu tofauti Iceland, Uganda, Tanzania na Oman.
Mazoezi ya Liewig
Mfaransa huyo anapenda kuona timu yake ikicheza kwa nafasi huku ikishambulia na kuzuia.
Liewig pia anasisitiza pasi bila kubutua na mpira lazima uanzishwe kutoka nyuma kwenda mbele. Pia ameweka mkazo katika kuhakikisha kuwa wacheza wanafanya vitendo kwa umakini.
"Kila mmoja anapaswa kuwa makini na majukumu yake ya uwanjani." Kutokana na kutawanya nyota wake uwanja mzima, kumesaidia kuwasoma na bila shaka wanakuwa fiti zaidi.
Timu hiyo jana Ijumaa asubuhi ilifanya mazoezi katika Uwanja wa Seeb. Katika mazoezi ya jioni walifanyia katika uwanja unaomilikiwa na Klabu ya Fanja.
Wachezaji wengi wa Tanzania wamewahi kuchezea Fanja kama Ahmed Amasha, Yussuf Abeid, Talib Hilal, Hilal Hemed, Jamhuri Kihwelo, Abdulwakati Juma, Zahoro Salum, Innocent Haule, Madaraka Selemani na wengineo.
Ilipojichimbia Simba
Simba ipo katikati ya mji wa Muscat, Oman katika hoteli ya kifahari ya Al Madinah Holiday kwani kambi ya awali pembezoni mwa fukwe za bahari imebadilishwa. Katika hoteli hiyo kuna kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya mazoezi kwa wachezaji na mambo mengine, ina bwawa la kuogelea pamoja na gym ya mazoezi.
Umbali kutoka Uwanja wa Ndege wa Muscat hadi ilipo hoteli hiyo ni dakika 15 kwa usafiri wa gari.
Lakini pia kutoka katika hoteli hadi uwanja wa mazoezi wa Seeb ni kama dakika 18 kwa gari. Uwanja huo unamilikiwa na Shirikisho la Soka la Oman.
Hali ya hewa
Hali ya hewa ya hapa imetulia kabisa na haina tofauti kubwa na Tanzania kwani ni nyuzi joto 28. Kuna jua kwa mbali na baridi kidogo wakati wa jioni.
Wachezaji wengine
Simba imekuja kwa mafungu Oman, kwani wachezaji wengine walibaki kwa ajili ya Kombe la Mapinduzi na wengine walikuwa na kikosi cha Taifa Stars huko Ethiopia. Wachezaji waliobaki kwenye Kombe la Mapinduzi walitazamiwa kuwasili jana Ijumaa usiku wakiwa na Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange 'Kaburu'. Wachezaji waliokuwa Stars, Juma Kaseja, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Mrisho Ngassa, Amri Kiemba na Mwinyi Kazimoto walikuwa wanapaswa kuungana na kikosi hicho baada ya mechi ya jana kati ya Stars na Ethiopia huko Addis Ababa
Na wakati EMMANUEL Okwi na Mrisho Ngassa 'Anko' wameipotezea Simba nafasi ya kujipima na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Simba walipangiwa kucheza na Congo waliopiga kambi hapa kujiandaa na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, mwaka huu. Mechi hiyo ilitakiwa kuchezwa leo Jumamosi.
Kocha wa Simba, Patrick Liewig alifuta mchezo huo kutokana na kuwa na wachezaji wachache. Okwi anayeingarisha simba kutokana na kiwango chake, tangu alipokwenda kwao kwa mapumziko na kucheza mashindano ya Chalenji hajaripoti kambini na sasa imeripotiwa yupo Tunisia akifanya majaribio na klabu ya Esperance.
Ngassa pamoja na Amir Maftah, Juma Kaseja, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto na Shomari Kapombe wako na Taifa Stars huko Ethiopia.
Kocha wa zamani wa Simba, Talib Hilal, ambaye ni mwenyeji wao hapa, alisema Congo, ambayo inaongozwa na nahodha wake, Tresor Mputu walitaka mechi hiyo leo Jumamosi.
Hata hivyo, Simba ina wachezaji wanane tu hapa; Felix Sunzu, Abel Dhaira, Nassor Said 'Cholo', Haruna Shamte, Kigi Makassy, Salim Kinje, Haruna Moshi 'Boban' na Ramadhani Chombo 'Redondo'.
Wachezaji wengine walibaki Zanzibar kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi kabla ya kuondolewa hatua ya nusu fainali na Azam FC.
Simba watacheza mechi ya kwanza dhidi ya timu ya Olimpiki ya Oman, Jumanne ijayo. Watajipima ubavu na Suwqi Januari 18 na watamaliza na Fanja FC.
No comments:
Post a Comment