Tenga akizungumza leo TFF |
Na Boniface Wambura, Dar es Salaam
RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
amesema kwamba amekamilisha ajenda yake ya kulijenga shirikisho hilo kuwa taasisi,
kwa kuweka mifumo bora ya uendeshaji ikiwemo kutengeneza katiba mpya na kanuni,
hivyo hatagombea tena wadhifa huo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari
24 mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye ofisi za TFF leo,
Rais Tenga amesema wakati anaingia kwenye uongozi mwaka 2004 ajenda ilikuwa na
kuijenga TFF kama taasisi kwa kuweka mifumo ya uendeshaji ikiwemo kutengeneza
katiba na kanuni, jambo ambalo limefanyika.
“Wajumbe wamekuwa wakiniuliza Rais vipi? Mimi hapana.
Nilishafika pale pa kufika. Tulipoanza wakati ule ilikuwa ni kujenga taasisi.
Na kazi hiyo tumeifanya. Tulipoingia mwaka 2004 hiyo ndiyo ilikuwa ajenda,”
amesema Rais Tenga.
Amesema walitengeneza Katiba, vyombo huru vya kufanya uamuzi,
kuongeza wigo wa wapiga kura ambapo hivi sasa kwenye mpira wa miguu hakuwezi
kutokea migogoro, hata ikitokea kuna mfumo wa kuidhibiti.
Rais Tenga ameishukuru Sekretarieti ya TFF, Kamati ya
Uchaguzi ya TFF, kamati za uchaguzi za wanachama wa TFF na vyama wanachama wa
TFF kwa hatua iliyofikiwa katika uchaguzi ambapo mikoa yote imekamilisha
uchaguzi na kubaki vyama shiriki pekee.
Ametoa mwito kwa wadau kujitokeza kugombea uongozi TFF, kwani
baada ya kujenga taasisi ajenda iliyobaki ni mpira wa miguu wenyewe ikiwemo
nini kifanyika ili mpira uchezwe katika maeneo mbalimbali.
“Tumeshatengeza mfumo, sasa ni kuangalia jinsi ya kuendeleza
mpira. Changamoto ni tufanye nini ili mpira uendelee. Tunataka watu wengine
wabebe hiyo ajenda ili tuangalie tunakwendaje mbele,” amesema.
Pia amesema ushirikiano ambao amepata kwa wapenzi na wadau wa
mpira wa miguu ni wa ajabu. Vilevile ameishukuru vyombo vya habari, Serikali,
klabu, wadhamini na wafadhili kwa mchango wao katika uendeshaji wa mpira wa
miguu nchini.
Wakati huo huo, wadau 19 wamechukua fomu kuwania nafasi mbalimbali
za uongozi katika uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
unaotarajiwa kufanyika Februari 24 mwaka huu.
Fomu hizo zimeanza kutolewa leo (Januari 14 mwaka huu) ambapo
wawili wamechukua nafasi ya Makamu wa Rais wakati waliobaki wanaomba ujumbe wa
Kamati ya Utendaji wakiwakilisha kanda mbalimbali.
Waliochukua fomu za umakamu wa rais ni Wallace Karia na
Ramadhan Nassib. Wote ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF inayomaliza muda
wake.
Waliochukua fomu za Ujumbe ni Shaffih Dauda, Athuman Kambi,
Hussein Mwamba, Stewart Masima, Yusuph Kitumbo, Mugisha Galibona, Vedastus
Lufano, Twahili Njoki, Charles Mugondo, Elley Mbise, Farid Nahdi, Ayubu
Nyaulingo, Nazarius Kilungeja, Epaphra Swai, Khalid Abdallah, James Mhagama na
Selemani Bandiho.
Katika hatua nyingine, TFF imeupongeza uongozi mpya wa Chama
cha Soka Katavi (KAREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana
(Januari 13 mwaka huu).
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama
hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa KAREFA walivyo na imani kubwa
kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Katavi.
TFF imeahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya
Utendaji ya KAREFA chini ya ukatibu wa Peter Hella aliyeibuka mshindi katika
uchaguzi huo uliofanyika ukumbi wa DC mjini Mpanda kwa kumshinda Emmanuel
Chaula kwa kura sita dhidi ya mbili.
TFF imesema uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa
ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Katavi kwa
kuzingatia katiba ya KAREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu
yake.
TFF pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya KAREFA na
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu
wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa ni Hella (Katibu), Elias Mande
(Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF) na Deo Bakuba (Mwakilishi wa Klabu TFF). Nafasi ya
Mwenyekiti haikuwa na mgombea wakati Mawazo Maso aliyekuwa mgombea pekee wa
nafasi ya Makamu Mwenyekiti alipata kura nyingi za hapana. Nafasi zilizo wazi
zitajazwa katika uchaguzi mdogo.
(Boniface Wambura ni Ofisa Habari wa TFF)Baada ya kushuka mascut oman ngassa na wenzake |
No comments:
Post a Comment